MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO, NI CHANZO KIKUU CHA SARATANI YA KOO?
Saratani imeendelea kuwa
tishio hapa nchini huku hofu ikiendelea kuikumba jamii kutokana na
wataalamu wa afya kushindwa kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo hatari.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha ongezeko
la saratani ya mdomo na koo kwa kiasi kikubwa kutoka kesi 167 mwaka 2006
hadi 277 mwaka 2012. Mkurugenzi wa Idara ya Kinga....
Ocean road, Julius Mwaiselage
anaeleza kuwa watanzania wasipende kuiga mambo ambayo si sahihi bila
kujua madhara yake kama kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo. “Saratani ya
mdomo ipo, na nyingine zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk Mwaiselage
Tafiti za saratani
Tafiti mbalimbali zimewahi
kufanyika nchini na kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani ya
mdomo.Utafiti uliofanywa na Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia
cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini aina za saratani
1,594, kati ya hizo 509 zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003 pekee.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati ya saratani 509 za mdomo, saratani
242 zilisababishwa na Virusi vya Human Papiloma ambavyo hutokana na
zinaa. “Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya HPV husababishwa na magonjwa
ya zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya aina hiyo, imetokana na
zinaa,” anasema Dk Mosha.
Wanaume waathirika zaidi wa Saratani
Takwimu hizo ni zile
zilizopatikana kwa watu waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika Mkoa wa
Dar es Salaam pekee. Dk Mosha anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa
zaidi na saratani ya mdomo ambapo kwa hapa nchini, asilimia 53 ya
wanaume waliofika MNH kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua saratani
hiyo, huku wanawake wakiwa ni asilimia 47. Utafiti kama huo ulifanywa
pia na Dk Amos Mwakigonja, mkuu wa Idara ya Patholojia katika Chuo Kikuu
cha Tiba cha Muhimbili (MUHAS).
Dk Mwakigonja alifanya utafiti
wa saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo wagonjwa 78
walibainika na saratani hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za
mdomo zipo za aina nyingi na zimetofautiana kulingana na visababishi
vyake,” anasema Dk Mwakigonja. Katika utafiti wake Dk Mwakigonja
alibaini kuwa wanawake wengi walikuwa na saratani ya mdomo aina ya
Kaposi’s Sarcoma kuliko wanaume.
Hata hivyo, utafiti huo
ulionyesha kuwa asilimia 50 ya wanaume walikuwa na saratani ya mdomo
hatari zaidi (systemic) kuliko wanawake ambao ni asilimia 37.
Mapenzi kwa mdomo husababisha maradhi
Dk Mwakigonja anasema kuwa
mapenzi yoyote kwa njia ya mdomo lazima yasababishe maradhi ya zinaa
iwapo mmoja ameambukizwa. Pia anasema kwamba sampuli nyingi za wanaume
wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) zilibainika na
saratani ya mdomo. Utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa Shahada ya
Uzamivu ambao ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa saratani ya mdomo
walikuwa ni wanaume wenye umri wa miaka kati ya 38 na kuendelea na
wanawake ni 31.
Ufatiti wa WHO Tanzania
Shirika la Afya Duniani (WHO)
pia lilifanya utafiti mwaka 2010 nchini kwa kushirikiana na Kituo cha
Taarifa za HPV, ambapo ilibainika kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na
mdomo nchini zinasababishwa na ufanyaji wa mapenzi kwa njia ya mdomo.
Taarifa hizo za WHO zinaeleza
kuwa wanaume 747 hugundulika na saratani ya mdomo kila mwaka wakati
wanawake 472 hubainika na saratani hiyo pia. Wakati huohuo, wanaume
wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo ni 444, kwa mwaka na
wanawake ni 270, kwa mwaka. Utafiti wa WHO umebaini kuwa saratani ya
mdomo inashika nafasi ya sita katika aina 24 za saratani 24
zinazoisumbua zaidi Tanzania.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa
wanaume wanaoathirika zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka 15 na 55,
ambao tayari wameshaanza kujihusisha na ngono. Kama maradhi mengine ya
kuambukiza, Virusi vya HPV huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka kwa
wanawake kwenda kwa wanaume kuliko kutoka kwa wanaume kwenda kwa
wanawake. Utafiti huo uliodhaminiwa na mfuko wa Bill na Melinda Gates na
Kituo cha Saratani na Mpango wa Utafiti wa Taasisi ya ICO unaeleza kuwa
mitandao ya kijamii na picha za ngono ndiyo chanzo cha watu wengi kuiga
ufanyaji wa mapenzi ya aina hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The
New York Times, tafiti zimefanyika na kubaini kuwa asilimia 70 ya
wagonjwa wanaobainika na saratani ya koo na mdomo duniani, husababishwa
na Virusi vya Human Pappiloma vinavyotokana na magonjwa ya zinaa.Tafiti
hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wanaogundulika na saratani hiyo ni
wanaume wenye umri wa kati, wenye uwezo wa kifedha, wasiovuta sigara
wala siyo walevi waliokubuhu.
Utafiti huo ulibaini kuwa
wanaume wapo hatarini zaidi kupata saratani ya koo inayosababishwa na
Virusi vya HPV. Miaka ya 80, idadi ndogo ya watu waliougua saratani ya
koo walihusishwa na maambukizi ya Virusi vya HPV. Kihistoria, watu
waliobainika na ugonjwa huo, ni wenye umri wa miaka 70 kwenda juu ambao
walikuwa ni wale walevi waliokubuhu na wavuta sigara.
Ilielezwa kuwa Virusi vya HPV
vipo kwa wingi kiasi ambacho watu wazima wanaojihusisha na ngono ya aina
yeyote ile, huweza kupata maambukizi ya zinaa hata kama siyo saratani.
Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani isababishwayo na virusi vya HPV ni
rahisi kuitibu kuliko saratani ya koo isababishwayo na tumbaku au pombe
kali.
Virusi vya HPV ni nini?
Kwa jina la jumla, saratani ya
koo au mdomo huitwa saratani ya kichwa na shingo. (Neck and Head
Cancer) HPV ni miongoni mwa virusi hatari zaidi duniani visababishwavyo
na magonjwa ya zinaa na vinaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili.
Zipo aina zaidi ya 120 za HPV, baadhi huweza kuzalisha usugu (warts)
ambazo si saratani katika sehemu za siri, mikononi na miguuni.
Maambukizi ya HPV hufanyika kwa urahisi, hata kwa kugusana ngozi au
majimaji, huku maambukizi mengine yakisababishwa na ngono.
Virusi hatari na
vinavyosababisha saratani ni HPV-16, HPV-18, HPV-31 na HPV 45. Aina hii
ya Virusi vya HPV husababisha saratani ambapo uvimbe waweza kujitokeza
kwa ndani na unaweza usionekane ukilinganisha na vivimbe vingine vya
saratani. Wataalamu wanasema HPV-16 na HPV-18 inahusishwa zaidi na
saratani ya shingo ya kizazi na endapo mapenzi kwa njia ya mdomo
yatafanywa na mtu mwenye uambukizo huu ni rahisi kuambukizwa.
0 comments:
Post a Comment